Barua 59; Soma Vitabu, Jua Falsafa Ila Wekeza Nguvu Nyingi Kuishi Kile Ulichosoma
Utapimwa Kwa Matendo na Si Kauli
Kinachokubadilisha maisha ni hatua unazochukua au matendo unayotenda au tabia fulani. Haitoshi kujua mambo pekee ila kuingia kuyakabili moja kwa moja ndo kupe uzito mkubwa. Uzoefu unaopata kwa kufanya kitu na kusikia juu ya kitu ni hali mbili tofauti. Kuwa na nadharia pekee bila matendo haimsaidii mtu kuelewa mambo katika uhalisia wake. Kuna kundi kubwa la watu ambao wanajua wanayopaswa kufanya ila hawafanyi. Maarifa pekee bila kutendea kazi hayana faida au makali.
Falsafa inahimiza zaidi ukishajua unachopaswa kufanya basi unaanza mara moja kuishi, kukabiliana na hali na kuwa tayari kupimwa na matukio ya maisha. Nguvu nyingi inahitajika kuishi yale uyajuayo kuliko kutumia nguvu hizo kujaa nadharia bila kwenda kukabiliana na hali zenyewe moja kwa moja. Vitabu vikupe tu nuru ya mambo ila kutenda au kushiriki kuchukua hatua kukabiliana na maisha ndio njia ya falsafa yenyewe ya kupimwa kama kweli u tayari kusimama katika misukosuko ya maisha.
Siku zinapoisha unahitaji kuondoka na uzoefu wa mambo ambayo maishani utapitia. Uzoefu ambao unakusanya kupitia kuishi hali mbalimbali katika maisha ni hazina na utajiri wa kweli unaojaa hekima na miongozo ya kweli kwa watu. Watu ambao wanapitia vitu moja kwa moja huwa wana uzoefu mkubwa wa mambo kuliko wale ambao husikia tu vitu vinavyokua au kusoma pekee bila kujisukuma kupitia hali hizo.
Hakikisha kila unachosoma basi chukua sehemu fulani ya ulichosoma na kitafutie namna anza kukiishi na upate uzoefu wake moja kwa moja. Unavyojipa nafasi hizi za kuishi unachojifunza unajengeka kiuzoefu, unakomaa kiakili na unajua uhalisia wa maisha ulivyo. Umesoma kitabu kimekupa maarifa kuhusu falsafa basi chagua kati ya yale ulojifunza yaishi na ujipime namna unavyoweza kuishi kwa ulichojifunza. Uwekezaji wa nguvu nyingi katika kutenda utakuzalia matokeo makubwa zaidi kuliko kujua pekee bila kuchukua hatua.
Dkt. Raymond N Mgeni
+255 676 559 211